Kwa mujibu wa shirika la habari la kimataifa la ahlul-bayt (as) - ABNA- Sayyidat Zainab (as) alitekeleza jukumu muhimu la kimawasiliano na uhamasishaji baada ya tukio la Karbala, kwa kufichua upotoshaji wa propaganda za umawi, kuathiri maoni ya umma na kuhifadhi ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein (as) kwa vizazi vijavyo.
Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Sayyidat Zainab (as) alichukua nafasi muhimu katika kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein (as) baada ya Tukio la kusikitisha la Karbala, kupitia hotuba zake zenye nguvu, ufafanuzi wa ukweli na kukabiliana na upotoshaji wa vyombo vya propaganda vya utawala wa umawi.
Kufichua Upotoshaji wa Propaganda za Bani Umaiyya
Miongoni mwa mihimili muhimu ya mawasiliano ya Kizainabiy ni kufichua upotoshaji wa habari. Sayyidat Zainab (as) alikabiliana na propaganda za Umawi (Bani Umaiyya) zilizojaribu kuwapotosha watu na kuwaonyesha mateka wa familia ya Mtume Muhammad (saww) kama watu waliotoka katika Dini (kwa maana: Watu walio dhidi ya Dini). Kupitia kauli zake zenye ujasiri, alifichua ukweli wa waliomuua Imam Hussein (as) na kuonyesha wazi kwamba uhalifu huo ulifanywa na wafuasi wa utawala dhalimu.
Kuathiri na Kubadilisha Maoni ya Umma
Sayyidat Zainab (as) alichangia kwa kiasi kikubwa kuathiri maoni ya umma. Hotuba yake mjini Kufa ilitikisa nyoyo za watu na kuwafanya watambue ukubwa wa usaliti na kosa walilolifanya dhidi ya Imam Hussein (as) na watu wa nyumba ya Mtume (saww).
Hotuba ya Sham (Syria) na Mshtuko wa Kisiasa
Hotuba ya Sayyidat Zainab (as) katika Ikulu ya Yazid bin Muawia mjini Damascus ilisababisha mshtuko mkubwa wa kisiasa na kijamii, na kuwafanya watu wengi kuanza kuuelewa ukweli wa Tukio la Karbala na kuonyesha huruma na mshikamano wao kwa Ahlul-Bayt (as).
Kuhifadhi Ujumbe wa Mapambano ya Imam Hussein (as)
Sayyidat Zainab (as) alitekeleza jukumu muhimu la kuhifadhi ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein (as). Kwa uelewa wake, ujasiri na ujumbe wake wa wazi, alihakikisha kwamba malengo ya mapambano ya Karbala hayapotei wala kufunikwa na propaganda za watawala.
Kuifanya Kadhia ya Imam Hussein (as) kuwa Hai katika Historia
Kwa msingi huo, ujumbe wa Sayyidat Zainab (as) uliweka msingi wa kuifanya kadhia ya Imam Hussein (as) kuwa hai katika historia, na kuifikisha kwa vizazi vijavyo kama ujumbe wa kupinga dhulma, kutetea haki na kusimama dhidi ya upotoshaji.
Sheikh Dr.Reihan Yasin
Jamiatul Mustafa (s) - Tanzania.
18 / 07/ 2026

Maoni yako